Wednesday, 24 April 2024

MDAHALO WA KITAIFA WA WANAWAKE NA MUUNGANO KUFANYIKA KESHO MLIMANI CITY JIJINI DAR ES SALAAM

 Rais wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Samia Suluhu Hassan

...............................

Na Dotto Mwaibale

WAKATI tukielekea  Maadhimisho ya siku ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yatakayofanyika Aprili 26, 2024, Umoja wa Wanawake Tanzania ( UWT ) umeandaa mdahalo wa Kitaifa wenye Dhima ya Nafasi ya Wanawake ndani ya miaka 60 ya Muungano. Tulipotoka, Tulipo na Tunapoelekea litakalofanyika kesho Aprili 25, 2024 Ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Taifa wa Umoja huo Mary Chatanda akizungumzia kuhusu mdahalo huo alisema maandalizi yote yapo tayari na kuwa utakuwa na mada mbalimbali zitakazo tolewa na wabobezi wa masuala ya kisiasa nchini ambapo mgeni rasmi atakuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussen Ali Mwinyi.

Chatanda aliwataja wabobezi hao ambao pia walishika nafasi za juu za uongozi hapa nchini kuwa ni Profesa Palamagamba Kabudi ambaye atatoa mada inayohusu Historia ya Nafasi ya Mwanamke katika Muungano na Balozi Amina Salum Ali ambaye atatoa mada inayoelezea Mwanamke na uongozi, faida za Muungano katika ukuaji wa kijinsia (kisiasa, kiuchumi na kijamii)

Aliwataja watoa mada wengine kuwa ni Mama Anna Abdallah ambaye ataelezea mchango wa UWT katika Muungano, Profesa Ruth Meena ambaye atatoa mada inayozungumzia matarajio ya miaka 60 ya Muungano, Nafasi ya mwanamke katika uongozi, ambapo pia Mama Zakia Meghji na viongozi wengine maarufu na wastaafu watakuwepo.

Mwenyekiti wa UWT Taifa, Mary Chatanda ambaye ametajwa kuwa ni moto wa kuotea mbali usiozimika na timu yake ndio waliouandaa mdahalo huo anatumia nafasi hiyo kuwaalika wananchi  kwenda kuhudhuria mdahalo huo ambao ni muhimu kwa muktaza wa Taifa letu la Jamhuri  ya Muungano wa Tanzania na kuwa litaanza Saa 2: 00 asubuhi.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussen Ali Mwinyi.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania ( UWT ) Taifa, Mary ChatandaMakamu Mwenyekiti wa UWT Taifa, Zainabu ShomariProfesa Palamagamba Kabudi

Profesa  Ruth Meena.
Balozi Amina Salum Ali.
Mama Anna Abdallah.
Mama Zakia Meghji.



 

No comments:

Post a Comment